Thursday, March 16, 2017

Siku ya Wanawake yafana City Harvest

WWK katika picha ya pamoja na Wachungaji
Maadhimisho ya siku ya wanawake katika kanisa la City Harvest lililopo Bahari Beach jijini Dar es Salaam yamekuwa na mvuto wa kipekee. Idara ya wanawake kanisani hapo (WWK) ambayo ndiyo iliongoza maandalizi ya maadhimisho ya siku hiyo, ilikuwa na mengi ya kuwasilisha ikiwa ni kuonyesha mchango wa wanawake katika kulijenga kanisa na kuujenga Ufalme wa Mungu kwa ujumla.

Mhubiri wa jumapili hiyo alikuwa Mchunagji Rose Mavika ambaye alisisitiza juu ya uchaji Mungu kama sifa kuu ya mwanamke katika kanisa. Neno kuu la siku ya wanawake mwaka huu lilitoka kitabu cha Mithali 31:30 “Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa.”

Mama Rosemary Mavika akihubiri City Harvest siku ya Wanawake

Mchungaji Mavika aliendelea kusisitiza kuwa anayemcha Bwana ni wa tofauti, ana Roho njema kutoka kwa Bwana, na ikiwa mwanamke atakuwa mcha Mungu, basi familia, jamii na taifa zima litaambukizwa kumcha Bwana, kama ilivyokuwa ushuhuda kwa maisha yake.



Katika kuendelea kumcha Bwana, Mchungaji Mavika alitaja mambo makuu matano ya kuendelea kuyashika, ambayo ni Maombi, Neno la Bwana, Utoaji, Kukusanyika pamoja na Kushuhudia.

Katika maombi, mwanamke ni lazima kuibeba familia na jamii yake, na kuacha kufuata watu kama mke wa Ayubu (Ayubu 2:9), Safira mke wa Anania (Matendo 5), na pia Delila, ambao kutoka kwao hatujifunzi mambo mema.

Maombezi yakiongozwa na Mchungaji Mavika
Katika maombi ni muhimu kujitakasa kwani kufanya hivyo ni kama binti anayejiandaa kumpokea mchumba wake.

Vilevile Mchungaji Mavika alisisitiza kuhusu kusoma na kujifunza Neno la Bwana (Joshua 1:1-9; Wakolosai 3:16) ili kuendelea kusikia kutoka kwa Mungu.

Pamoja na hayo, msisitizo ulikuwepo kwenye utoaji sadaka na zaka (Malaki 3:7-10; Malaki 1:6-14; Kutoka 25) Kukusanyika pamoja (Waebrania 10:25) kwenye ibada za pamoja kanisani, welcome groups na kusanyiko la nyumbani.


Mchungaji wa kanisa Matilda na Mchungaji Kiongozi
Yared Dondo wakikata keki kuadhimisha siku ya wanawake
Wanawake pia wanapaswa kuwa washuhudiaji, wahubiri wa Injili. Lakini juu ya yote, uhitaji wa kujazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu wa Mungu afanyaye kazi ndani yetu (Luka 24:49; Matendo 1:8)

Katika shughuli nyingine, wanawake walithamini mchango wa watu mbalimbali katika huduma yao ikiwemo Wachungaji na viongozi wao kwa kuwapa zawadi kama sehemu ya kuwashukuru na vilevile kuchangia gharama ya ununuzi wa samani kwa ajili ya ofisi ya Mchungaji wa kanisa la City Harvest ambalo limehamia katika jengo lake jipya Bahari Beach

Wanawake wa City Harvest pia waliongoza ibada ya siku hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na nyimbo maalumu, shairi na igizo kama sehemu ya maadhimisho hayo muhimu ya kila mwaka.
Mchungaji wa WWK Dk. Bertha Kipilimba akikabidhi zawadi
kwa Mchungaji Kiongozi Architect Yared Dondo
Mstari wa mwaka kwa WWK: Mithali 31:30 “Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa.”

No comments:

Post a Comment