Tuesday, January 10, 2017

MWIMBAJI WA WIKI - JOSHUA SILOMBA

LEO TUKO NA MCHUNGAJI JOSHUA SILOMBA
Mchungaji Joshua Silomba
Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Joshua Silomba: Naitwa Joshua Silomba wakati mwingine huwa naitwa Pastor Joshua kutokana na huduma yangu ya kichungaji.

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Joshua Silomba: Nimeokoka, ninaabudu kanisa la T.A.G Toangoma na pia ninatumika kama Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo (Mchungaji wa Vijana/Sifa na Kuabudu).

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi ulianzia?

Joshua Silomba: Nakumbuka nilianza kuimba nikiwa mtoto kabisa kule nyumbani Vwawa, Mbozi. Baba yangu alikuwa Mchungaji na familia kwa ujumla ni ya Kikristo hivyo muda mwingi tulikuwa tukiimba nyumbani na kanisani pia hasa kwenye Sunday School. Nilikigundua zaidi kipaji changu cha kuimba nilipoanza kusoma Shule ya Sekondari miaka ya 2000, nilipofika kidato cha pili niliendelea zaidi kugundua uwezo wangu wa kuongoza ibada (kuimbisha), kupiga muziki na pia kutunga nyimbo. Mwaka 2003 nilikabidhiwa rasmi jukumu la kufundisha kwaya ya kanisa la TAG Mji Mkuu nikiwa Morogoro na tangu hapo nimeendelea kumtumikia Mungu katika maeneo yote niliyoyataja hapo juu (Kuongoza ibada, kupiga muziki, kutunga nyimbo zangu binafsi na kwaya na pia kufundisha kwaya na timu za kusifu na kuabudu).

Joshua akiiongoza ibada na sifa kanisani
Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa albumu yoyote? Majina ya albamu?

Joshua Silomba: Nimewahi kutoa albumu mwaka 2010 iliyoitwa MUNGU WETU HASHINDWI (audio) na kwa sasa nina albumu nyinginei itwayo JAMBO JIPYA (audio) ambayo niliitoa rasmi tarehe 04.12.2016.

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?

Joshua Silomba: Kwa kweli napenda nyimbo zangu zote kwa kuwa kila wimbo umebeba ujumbe maalumu na pia sababu maalumu ya kutungwa kwake. Hivyo, kila wimbo una mguso wa kipekee napozisikiliza na kuziimba pia.

Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?


Joshua Silomba: Kwa sasa sina msambazaji wala mtu anayesimamia kazi zangu, labda kwa hapo baadaye.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Joshua Silomba:    Kwa Tanzania ni wengi wanaonivutia katika muziki wa Injili hususani wanaoimba nyimbo za sifa na ibada. Kwa nje ya nchi kwa sas anapenda sana kumsikiliza na kumfuatilia William McDowell.

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Joshua Silomba: Mafanikio ninayoyaona kwa sasa ni kupanuliwa zaidi kwa wigo wa kihuduma, watu wengi zaidi wanaendelea kunifahamu na kufuatilia ninachofanya katika huduma yangu. Pia naendelea kuwafahamu na kukutana na wadau mbalimbali wa muziki wa Injili kama vile wazalisha muziki (producers), waongoza video (video directors) na waimbaji ambao wananipa changamoto ya kufanya kazi katika ubora na viwango vya hali ya juu.

Joshua Silomba
Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Joshua Silomba: Changamoto ni nyingi ila kwa uchache, nimepata sana changamoto ya kifedha katika kufanikisha malengo yangu ya kihuduma hivyo kufanya kazi zisizona viwango ninavyovitaka, ucheleweshwaji wa kazi studio au kupoteza kabisa (nimewahi kurekodi nyimbo ambazo hadi sasa sijazipata kwa miaka zaidi ya miwili, pia nimewahi kurekodi video ambazo sijawahi kuziona pasipo maelezo yanayojitosheleza). Changamoto nyingine ni kutopata ushirikiano kwa waimbaji wengi waliotangulia kwenye huduma hii ya uimbaji na mwisho, mfumo wa vyombo vya habari wa Tanzania (Redio, TV, nk) hautii sana moyo hasa kwa waimbaji wanaoanza huduma hivyo ziko nyakati ambazo nilikatishwa sana tamaa na mfumo huu.

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Joshua Silomba: Muziki wa Injili Tanzania unazidi kukua na changamoto inazidi kuwa kubwa hasa kwa upande wa ubora na viwango. Lakini pia kwa upande mwingine, muziki wetu umeingiliwa sana na mamluki, hivyo kusababisha waimbaji wengi hata wasio na shida kuonekana ni wababaishaji.

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Joshua Silomba: Nashauri waimbaji wanaojisahau na kujichanganya na mambo ya kidunia wajitambue na kurejea kwenye misingi ya Neno la Mungu ambalo linatuongoza kupita katika njia za haki na utakatifu. Zaidi wanatakiwa kutubu na kusimama kwenye kweli ili utumishi wao usiwe bure.

Joshua akiiongoza ibada na sifa kanisani
Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Joshua Silomba: Kama nilivyosema hapo awali, mimi ni Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la TAG Toangoma na nina wajibika zaidi kama Mchungaji wa Vijana na Sifa na Kuabudu (Youth/Worship Pastor). Najishughulisha pia na kilimo, ufugaji na biashara. Pia ni MC kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kikanisa.

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?

Joshua Silomba: Ninaishi Toangoma, Dar Es Salaam. Nina mke (Bertha) na mtoto mmoja (Doreen).

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Joshua Silomba: Tupendane, tuwe na umoja na pia tuishi maisha halisi ambayo yatamtukuza Mungu.

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Joshua Silomba: Waendelee kututia moyo na kutupa ushirikiano tunapotoa nyimbo.

Rejoice Blog: Ahsante sana Joshua Silomba kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Joshua Silomba: Amina! Nawashukuru pia Rejoice Blog kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuibua na kutangaza vipaji vya waimbaji wa nyimbo za Injili. Mungu awainue zaidi ili muwafikie watu wengi.


Kupata zaidi habari za huduma yangu kwa sasa natumia Facebook, page yangu natumia jina Joshua Silomba. Msomaji anaweza ku-like na ku-share na wengine ili waweze kujua habari mbalimbali zinazohusu huduma yangu. Pia YouTube kwa sasa nimeweka wimbo (audio) unaoitwa Jambo Jipya wanaweza kuusikiliza kwa kubofya link HAPA

Mawasilianoi zaidi piga: +255717387212/+255754773512

Mwisho kabisa napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa msomaji kutoa muda wake kufuatilia habari za muziki wa Injili kupitia Rejoice Blog.



~~~ UBARIKIWE ~~~


No comments:

Post a Comment