Monday, June 23, 2014

NAFSI ILIYONASWA na UZINZI na Frank Philip



Mtumishi Frank Philip
Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani …Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika” (Mithali 6:26 & 32,33).

Nimeona jambo hili, nami nikatafuta kujua kama kuna hekima ndani yake “men’s hearts can be shared, but women’s hearts replaces”. Maana yake: Moyo wa mwanaume ukipenda, waweza kupenda tena kwa wakati mmoja, ila moyo wa manamke ukipenda, humwondoa wa kwanza na kumpenda mwingine.

Ukitaka kuona kwa njia ya urahisi, jiulize ni kwanini mwanaume mmoja anaweza kuoa wake zaidi ya mmoja na maisha yakaenda? Na jiulize tena, je! Mwanamke anaweza kuwa na mpenzi wa nje ampendaye sana, na maisha yake ya ndoa/mahusiano yakawa sawa? Wote wawili: mwanamke na mwanaume, wana hatari ya kuingiliwa mioyoni mwao, japo kwa madhara tofauti.

Hii hali sio rahisi kuikubali katika mahusiano ya kawaida ambapo mtu anatoka nje ya ndoa/uhusiano kwa siri. Mara nyingi mtu afanyaye mambo hayo, hudhani yuko sawa, kumbe ameathirika kabisa. Ukitaka kujua ninachosema, angalia mambo ya kawaida kabisa ya kwenye ndoa/uhusiano kwa watu ambao mmoja au wote wamenaswa nafsi na kahaba. Mambo ya kawaida kabisa kwenye uhusiano/ndoa yanaanza kuwa kero, mzigo na ya kuchosha. Ukiona hii shida, usipambane na mtu kwa jinsi ya mwilini, shughulika na nafsi kwa sababu hapo ndipo penye shida.

Nitasema na wanawake sasa. Hii hali ya “replacement”, huwa haianzi mara moja. Huenda kwa awamu, na hatua mbali mbali, kuanzia hisia, matendo kisha ngono. Ndio maana mwanamke akitoka nje ya ndoa watu husema “amefika mbali”. Mara zote huanza na “nafsi kunaswa” na kahaba. Kama kuna mtego mbaya, ni kuacha nafsi yako inaswe. Kwenye nafsi ndiko kuliko na mawazo na maamuzi. Kama nafsi imenaswa, mara ZOTE mtu ataanza kuwaza tofauti, na kisha kufanya maamuzi mabaya. Ndio maana tunaonywa sana kwamba “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima” (Mithali 4:23). Ukitaka kuona uzima kwenye ndoa/uhusiano wako, linda sana moyo wako; ukitaka kuona mauti kwenye ndoa/uhusiano wako, achilia moyo wako uingiliwe.

Sasa kuna jambo la kuzingatia hapa. “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea.” (Mithali 23:7,8). Hii inamaanisha kwamba nafsi ya mtu huwa na uwezo wa kuona, au kujiona kwa namna fulani. Kwa lugha nyingine, MTAZAMO wa mtu hutokana na kile nafsi inachoona, na kisha huyo mtu hunena au kutenda kama aonavyo. Haiwezekani kwenda tena pamoja na mwenzako katika uhusiano/ndoa kama nafsi yake imenaswa kwa sababu ya kutofautiana kwa MITAZAMO. Mitizamo ikitofautiana, kila jambo ndani ya ndoa/uhusiano ni malumbano, mabishano na magomvi. Mara nyingi magomvi ya namna hii huwa hayana suluhu, kwa sababu nafsi zimenaswa. Kila mmoja anaona yuko sahihi na mwenzake ana makosa, kumbe mitazamo yao imeathirika.

Ona jambo jingine. “Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe” nafsi ya mtu kunasa, ni sawa na kuiacha huko mtaani wakati wewe uko nyumbani. Japo unafanya mambo hapa nyumbani, lakini “moyo wako haupo pamoja na mwenzako”; moyo uko kule kwa kahaba. Hii hali ikifikia hatua fulani huwa haifichiki tena. Mhusika hujua na mwenzake hujua, kwa maana mambo hubadilika kama jinsi nafsi (moyo) ulivyobadilika.

Ni vyema kujua mambo kadhaa yanayosababisha nafsi kunaswa. Jambo la kwanza ni kukaambali na Neno la Mungu, na la pili, ni kuishi maisha bila maombi. Mtu yeyote akikaa mbali na Neno la Mungu, anakuwa dhaifu kiroho. Hii hali inampelekea kuishi gizani. Daudi aliita Neno la Mungu “taa na mwangaza miguuni mwake”, ikimaanisha pasipo Neno, ni sawa na kutembea gizani. Kwa upande mwingine, Neno limeitwa “chakula cha roho/uzima”. Sasa fikiri, nafsi yenye njaa na dhaifu, kisha inatembea gizani! Hivi ndivyo ilivyo watu wengi hujikuta wameangukia shimoni ambamo hawakutarajia, kumbe walikuwa wanatembea bila taa (Neno), tena wakiwa na njaa ya siku nyingi (Neno) na dhaifu sana (bila maombi).

Nakupa shauri. Kama unajua nafsi yako imenaswa, na huwezi kabisa tena kufanya mapenzi ya Mungu kwenye uhusiano/ndoa yako, kimbilia kwa Yesu kuna dawa. Ukishangaa hapo, adui yako ni kama simba angurumaye; kazi yake ni kuharibu, kuchinja na kuangamiza.

 

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment