Monday, April 14, 2014

Mambo ya Msingi Kanisa linayoweza kupata kwa kujua/ kufahamu asili yake Sehemu ya II na Mwalimu Samwel Mkumbo

Mwalimu Samwel Mkumbo
Wiki iliyopita tulitazama kwa sehemu kama Utangulizi tu unaotupeleka kwenye Kujua kulingana na Somo hili juu ya MAMBO YA MSINGI KANISA LINAYOWEZA KUPATA KWA KUJUA/KUFAHAMU ASILI YAKE. Karibu tuendelee mtu wa Mungu,

 
Upo umuhimu sana wa kufahamu Asili ya Kanisa, na kama nilivyosema hapo mwanzoni ni kwamba si kwamba ninazungumzia Asili ya Kanisa kwa mtazamo wa Historia yake au mpangilio wa matukio yaliyotokea kwenye Kanisa tangu lilivyozaliwa, la hasha! Lakini nazungumzia Asili ya Kanisa kwa kutazama Uzao na Nafasi yake.

Hebu tutazame mifano michache itakayonisaidia kukuelekeza mambo ambayo ninataka nikuoneshe mtu wa MUNGU, katika mifano hii utaona mambo kadhaa ambayo yatafungua ufahamu wako umuhimu wa kujua Asili ya Kanisa kwa kutazama Uzao na Nafasi yake.

Habari za Wana wa Skewa.

Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.  (Matendo 19:13-16)

Sasa lengo kubwa si kukuonesha hadithi hiyo nzima, lakini kuna kipengele ambacho hakipo hapo kwenye hiyo mistari na si kwamba kimesahaulika kwenye hiyo mistari lakini hakipo kabisa,  lakini nataka nikitumie hicho hicho kipengele ambacho ukiangalia kwa undani hakipo ndicho nataka nitumie kukufundisha hapo. Kipengele chenyewe ni MAJIBU YA WANA WA SKEWA.

Maana ukiitazama hiyo mistari haioneshi wana wa Skewa wakijibu swali waliloulizwa na mtu mwenye Pepo, hata kidogo, na wala haituambii walishindwa kujibu wakakaa kimya, wala haisemi kwamba waliguna au waliinama chini au walisema jambo hata kama ni mioyoni mwao, ila Biblia inatuonesha kuwa baada ya yule mtu kuwauliza kitu kinachofuata aliwarukia wawili miongoni mwa wale waliokuwepo, na akawashinda nguvu akawaumiza lakini pia hakuwaacha waondoke hali wamevaa nguo zao.

TAZAMA NAMI:

Tuseme kwamba hii ni kesi, na huyu mtu mwenye pepo ametoa Hukumu kwa wana wa Skewa, na hukumu yenyewe ni ya kuwapiga na kuwaumiza na kuwachania nguo zao, kwa kosa la kutaka kumtoa mahali bila ya ruhusa tena bila ya kuwa na mamlaka au hati ya kumtoa lakini zaidi KWA KOSA LA KUWAULIZA SWALI NA WAO KUKOSA JIBU.

Tazama tena:

Kwamba huyu mtu mwenye pepo hana akili sawasawa ndio maana aliwapiga na kuwararua na kuchana mavazi yao, kwa hiyo alifanya hayo kwa kuwa alikuwa amechanganyikiwa na hivyo hata hilo alilolifanya alilifanya katika hali ya kutokujitambua kabisa.

Kimsingi wana wa Skewa hawakuwa na Jibu la kumjibu Yule pepo kwa kuwa HAWAKUWA WANAJUA WAO NI KINA NANI KATIKA HAYO MASHINDANO na ndio maana walikosa Jibu.

Lakini biblia inatuwekea mambo kadhaa ambayo ni muhimu tukayapitia  na kuyaangalia yanaweza kutupa mwanga wa namna hiyo kesi ilivyoenda na kuona maana halisi ya kukupa mfano huu.

Kwanza kabisa hata kama Wana wa Skewa hawakumjibu yule mtu mwenye pepo au katika mahojiano yao Biblia haikuonesha ni nini wa Wana wa Skewa walijibu lakini mwanzoni mwa maelezo ya tukio hilo Biblia inatujibu majibu ya swali alilouliza mtu mwenye pepo.

Kimsingi SIFA ZA WANA WA SKEWA ndizo majibu ya swali la yule mtu mwenye pepo alipowauliza wao ni akina nani. Sifa za wa wana wa Skewa zimeelezwa kuamzia tu ule mstari wa 13 biblia inasema hivi;

Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo,….. lakini pia kuna jambo ambalo linaoneshwa tena juu ya sifa za wana wa Skewa katika mstari ule wa 14…. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo…..

Biblia imetuonesha mambo kadhaa hapo juu ya sifa za wana wa Skewa, kwanza walikuwa ni Wayahudi, lakini walikuwa ni watu wa Kutanga-tanga, maana yake hawana Kikao maalumu, hawana Imani thabiti mioyoni mwao, yaani hawana msimamo wala haijulikani misingi yao wala dhehebu lao wanaloabudu, tena walikuwa ni Wapunga mapepo yaani ni kama Waganga wa Kienyeji zaidi ya yote WALIKUWA WATOTO WA KUHANI MKUU. Nisikilize kijana mwenzangu, nisikilize mtu wa Mungu kuwa mtoto wa mtumishi au kuwa mtoto wa Mchungaji au Mke au Mume wa mtumishi, au Kusali Kanisa au Dhehebu Fulani sio Tiketi hata kidogo ya kukufanya uwe mtu wa aina Fulani mbele za MUNGU au shetani kama Hujaookoka.

Sasa hebu pata picha mtu ameshakuwa wa Kutanga-tanga, tena wakati huo huo tunae ibadani, akitoka au hata akiwepo Imani yake au mawazo yake hayapo, hayana utulivu. Imani yake haieleweki, mtu kama huyo asitegemee kuijua asili yake maana hajijui yeye ni wa kutoka wapi na anakwenda wapi ndio maana anatanga-tanga kwa sababu mtu anayejua anakotoka na anakokwenda hawezi kutanga-tanga.

Kwa hiyo basi yule mtu mwenye pepo alipouliza swali, ni lazima wana wa Skewa wanganyamaza kwa sababu wasingeweza kujieleza kwa kutumia Sifa zao, yaani waseme ya kwamba sisi ni Wayahudi, watoto wa Kuhani Mkuu, lakini kwa Upande wa Imani sisi ni watu wa Kutanga-tanga, na kwa upande wa Huduma sisi ni Wapunga pepo. Hata kama ungelikuwa ni wewe au ni mimi basi usingeweza kujibu swali kama hilo, lakini pia wasingeweza Kuongopa.

Labda tuseme wangesema wao ni watumishi wa Mungu aliye Hai na wamekuja kumuamuru yule pepo atoke, Hakika WASINGEWEZA maana wangelikuwa WANAMDANGANYA SHETANI WAKATI YEYE NI BABA WA UONGO. Hivyo wana wa Skewa wakanyamaza, maana hawakujijua wao ni wa Uzao gani na wana Nafasi gani…..

 

Itaendelea….

 

No comments:

Post a Comment