Monday, April 29, 2013

Benjamin Bukuku: Mchungaji anayehimiza Watanzania kufanya kazi

           
MAISHA ni safari ndefu, kila mtu anapoamua kufanya kazi huwa ana matarajio fulani.

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Mchungaji Benjamin Bukuku wa Huduma ya Kweli Itakuwaweka Huru yenye makao yake makuu Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mchungaji Bukuku alikuwa mfanyabiashara maarufu ghafla akajikuta akichunga kondoo wa bwana.

Katika mahojiano yake na gazeti hili Mchungaji Bukuku anaelezea safari yake ya kitumishi na mikakati aliyonayo kwa jamii ya Watanzania.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii katika ukumbi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, anasema ibada zake huwa zinatolewa ndani ya ukumbi wa chuo hicho kila Jumapili.

Anasema katika maisha yake hakutegemea kuwa mchungaji kwani alikuwa akijihusisha na ujasiriamali kazi aliyoipenda kwa sababu ilimuingizia kipato.

Anasema hakupenda kufanya kazi ya utumishi kwani miaka ya nyuma ilikua ni kazi duni, wachungaji wengi walikuwa na maisha magumu.

Anasema uchungaji haikuwa kazi ya kuitamani hususan kwa aliyekuwa akijishughulisha na biashara ingawa alipenda kusaidia kazi ya Mungu iweze kusonga mbele.

“Niliamini kwamba watu wakibadilika nchi itapona amani itadumishwa, taifa litakuwa na watu wema wenye hofu ya Mungu hivyo nilihakikisha katika kile ambacho Mungu ananijalia sehemu nasaidia kwenye Injili.

“Siku moja katika hali isiyokuwa ya kawaida mzigo wa kumtumia Mungu ulianza kuwaka moyoni, ghafla niliamua kufungua kanisa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Nilifungua kanisa lijulikanalo kwa jina la Amani liko chini ya Kanisa la Tanzania Assemblies Of  God ambalo nililianzisha miaka ya 1980 hadi hivi leo japo nimefungua makanisa mbalimbali vijijini malengo ambayo ninayo ni kuhakikisha nafungua makanisa mengi vijijini na kuyasaidia kwa hali na mali.

“Kwa miaka yote hiyo nimefarijika kuwapa ujumbe wa upendo Watanzania bila kujali tofauti za imani zao, mimi kwa muda mrefu nimekuwa mdau wa amani popote niendapo nahubiri upendo pamoja na amani kwa kutumia kauli mbiu yangu ya kweli,” anasema.

Akifafanua kauli mbiu hii ya “Kweli Itakuweka Huru” anasema Watanzania wanatakiwa waambiwe ukweli kwani wakishaufahamu watawekwa huru katika maeneo mengi ikiwepo magonjwa, uchumi na mambo mengine muhimu.

Lengo lake lingine anasema ni kukemea maovu na kuwaambia watu kuachana na maovu ikiwepo kuwahimiza watu kufanya kazi kwa bidii.

“Baada ya kufanikiwa sana mkoani Kilimanjaro sasa huduma yangu ya kweli itakuweka huru imefungua tawi jijini Dar es Salaam… Jumapili iliyopita ilikuwa ibada yetu ya kwanza mamia ya wakazi wa jiji waliweza kuhudhuria mkakati ukiwa ni kuwafikia maelfu ya wakazi,” anasema.

Mbali na hayo anasema kwa sasa kuna tatizo la maadili kwani miaka mingi kulikuwa na utamduni mzuri wa kupendana ambapo popote Tanzania ukienda hakuna mtu yeyote anayeweza kukuuliza wewe unatoka dini gani.

Hilo anasema lilitokana kwa sababu jamii iliishi kwa amani, upendo na undugu wa hali ya juu huku kila Mtanzania kuchagua imani anayoitaka.

Naungana na kauli ya Rais Mstaafu mzee wetu Ally Hasan Mwinyi kwa kauli yake iliyokuwa imejaa hekima za hali ya juu kwamba masuala ya imani hayalazimishwi Katiba iko wazi mtu aabudu dini yoyote anayoitaka mradi tu havunji sheria za nchi huu ndio utaratibu ambao tumeuzoa na umedumisha amani yetu.

Maoni yangu kwa serikali iliyoko madarakani kwa sasa isiogope mtu hata awe kiongozi wa dini kwani amani ikitoweka hakuna atayesalia bali watu watakimbia ovyo.

Kwa mujibu wa mchungaji Bukuku atahakikisha anahubiri ujumbe wa amani pamoja na upendo kwani ndio kazi ya viongozi wa dini.

“Viongozi wote wa dini ni vema tukaheshimu na kuzifuata sheria za nchi na tusitumie vibaya sheria ya uhuru wa kutoa maoni, nionavyo mimi kama atatokea kiongozi yeyote wa dini akatoa kauli inayohatarisha amani ya nchi serikali isimuogope imkamate na imfungulie mashtaka.

“Pia kauli za baadhi ya viongozi wa dini zinachochea hivyo ni vema serikali isiogope mtu hasa kwenye eneo la uvunjaji wa sheria,” anasema.

Anasema kwa sasa amejipanga kuhakikisha anaeneza ujumbe wa amani nchi nzima ambapo kwa kuanzia ameanza na Dar es Salaam, kisha ataendesha semina mbalimbali pamoja na makongamano ya kuhamasisha masuala ya amani na upendo.

Akizungumzia kazi za Rais Jakaya Kikwete anasema ni mchapakazi mzuri na ana nia njema ya kuwatumikia Watanzania.

“Sisi kama huduma tumekuwa tukimuombea sana yeye pamoja na baraza lake la mawaziri na serikali nzima kwa ujumla tatizo ninaloliona ni la kimfumo ameingia madarakani amewakuta watu wamezoea mfumo fulani ambao kuufumua ipo kazi,” anasema.

Kuhusu kusaidia jamii Mchungaji Bukuku anasema wamekuwa wakisaidia wajane na yatima ambapo kipo kitengo maalum kabisa katika kanisa lake kinachosaidia jamii.

Mbali na wajane anasema kitengo hicho pia huwa kinawasaidia wachungaji wa vijijini.

 

 

Source: Tanzania Daima

           

 

No comments:

Post a Comment